Vikosi vya usalama vya Cameroon vyawaokoa mateka 11 kutoka kwa wapiganaji wanaotaka kujitenga
2023-10-05 09:05:07| CRI

Takriban mateka 11 wanaoshikiliwa na wapiganaji wanaotaka kujitenga katika mkoa wa watu wanaozungumza Kiingereza wa Kaskazini-Magharibi nchini Cameroon wameokolewa na vikosi vya usalama.

Gavana wa wilaya ya Bui katika mkoa huo, Menyong Gilbert Sunday, alisema wanajeshi walifanya operesheni usiku kucha hadi Jumatano, na kupelekea kuwaokoa wanaume 10 na mwanamke mmoja waliokuwa wameshikiliwa mateka katika "kambi ya kigaidi" katika eneo la Kikaikom la tarafa hiyo.

Kwenye taarifa yake Sunday, alivipongeza vikosi vya usalama kwa "ujasiri na weledi" wao na kuwataka wakazi kuendelea kushirikiana na maafisa na askari katika jitihada za kuimarisha amani na utulivu katika eneo hilo ambapo wapiganaji wanaotaka kujitenga hufanya kazi mara kwa mara.

Watu hao wanaotaka kujitenga walitaka kuunda taifa huru katika mikoa miwili ya watu wanaozungumza Kiingereza ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi mwa Cameroon, na wamekuwa wakipambana na vikosi vya serikali katika mikoa hiyo tangu 2017.