Dawa za kuua wadudu za China zapiga jeki sekta ya kilimo nchini Kenya
2023-10-05 09:04:40| CRI

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Bidhaa za Kudhibiti Wadudu ya Kenya (PCPB), Fredrick Muchiri amesema dawa za kuulia wadudu za China, zinazochukua zaidi ya nusu ya soko la nchi hiyo, zina nafasi kubwa katika kukuza sekta ya kilimo nchini humo,

Bw. Muchiri ameyasema hayo kwenye kongamano la wadau kuhusu ulinzi wa mimea lililofanyika Nairobi nchini Kenya, ambapo ameeleza kuwa teknolojia ya China katika bidhaa za kudhibiti wadudu imefikia kiwango cha nchi zilizoendelea, na wakati mwingine hata kuzipita. Aidha amefafanua kuwa kwa upande wa ubora, ufanisi na usalama, zinakidhi viwango vya kimataifa vilivyowekwa kwa bidhaa za kudhibiti wadudu na zina thamani zaidi ya kiuchumi.

Muchiri alisema mapema mwaka huu, timu ya maafisa wa PCPB walitembelea China kuangalia michakato ya kutengeneza na kudhibiti ya makampuni ya kudhibiti wadudu nchini, na kugundua kuwa makampuni haya yanakidhi viwango vya kimataifa. Alibainisha kuwa wakulima wa kibiashara nchini Kenya hutegemea sana dawa za kuulia wadudu ili kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kila eneo na kupata faida nzuri kwenye uwekezaji wao.