Maonyesho ya biashara ya Uganda yavutia mashirika zaidi ya 900
2023-10-05 09:05:41| CRI

Maonyesho ya 29 ya biashara ya kimataifa ya Uganda (UGITF) yamefunguliwa mjini Kampala, na kuvutia mashirika 920 kutoka nchi takriban 30.

Maonyesho hayo yenye kauli mbiu ya “Kuhimiza ufanisi wa uzalishaji viwandani na biashara kupitia mageuzi ya kidigitali na uvumbuzi” yanafanyika kwenye uwanja wa maonyesho wa Shirikisho la Wazalishaji la Uganda (UMA) kuanzia tarehe 3 hadi 10 Oktoba.

Mwenyekiti wa Bodi ya Utendaji ya UMA Deo Kayemba alisema maonyesho hayo ni jukwaa kwa wafanyabiashara kutangaza mambo mapya ya uvumbuzi ya makampuni mapya na kuhimiza mtandao wa biashara. Maonyesho ya UGITF pia yanawapatia wawekezaji wa biashara na wadau husika fursa ya kufanya mawasiliano na kutafuta ushirikiano, hali ambayo inaweza kuharakisha matumizi ya teknolojia ya kidigitali na ufumbuzi wa kibunifu.