Kenya yazindua mipango ya kuvutia uwekezaji
2023-10-05 09:03:58| CRI

Kenya imeanzisha msururu wa miradi ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ili kusaidia kukuza uchumi, afisa wa serikali alisema.

Akiongea na wanahabari mjini Nairobi wakati wa uzinduzi wa Tamasha la sita la Manunuzi la Changamka linaloandaliwa na Chama cha Wazalishaji Kenya (KAM), mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Kenya (KenInvest), June Chepkemei, alisema serikali imeanzisha maeneo yanayojumuisha kaunti na viwanda ambayo wawekezaji wanaweza kutumia kuongeza thamani ya malighafi zinazopatikana nchini humo. Pia amesema wameanzisha maeneo maalum ya kiuchumi ambapo wawekezaji wanafurahia misamaha ya kodi na kurahisisha kupata vibali vya kufanya kazi.

Tamasha hilo, litakalofanyika Oktoba 31 hadi Novemba 4, litawaleta pamoja watengenezaji wa ndani na kuonesha bidhaa za ubora wa juu zinazotengenezwa Kenya, pamoja na Mkakati wa Nunua Kenya Jenga Kenya.

Kwa upande wake afisa mkuu mtendaji wa KAM, Anthony Mwangi, alisema wawekezaji wanaweza kusaidia nchi kukabiliana na pengo la matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa ndani ya nchi ikilinganishwa na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.