Kenya kuzindua kampeni mpya ya chanjo ili kukabiliana na mlipuko wa polio
2023-10-06 08:59:17| CRI

Wizara ya Afya ya Kenya imetangaza kuzindua kampeni ya pili ya chanjo ya polio.

Akiongea na wanahabari mjini Nairobi, Katibu Mkuu wa Idara ya Serikali ya Afya ya Umma na Viwango vya Taaluma katika Wizara ya Afya Mary Muthoni Muriuki, alisema kampeni hiyo ya chanjo itakayofanyika kwa siku tano itaanza Jumamosi, na kulenga kaunti 10 zilizo katika hatari kubwa zaidi za kaskazini mwa Kenya, kaskazini mashariki na mashariki mwa Kenya, katikati mwa Kenya, mkoa wa pwani na Nairobi.

Wizara hiyo ilisema kampeni hii inaashiria hatua muhimu katika juhudi zinazoendelea za kukabiliana na mlipuko wa polio uliozuka hivi karibuni katika Kaunti ya Garissa mashariki mwa Kenya mwezi Juni.

Muriuki alisema timu za uchunguzi zimegundua wagonjwa wengine wawili wa polio, na kufanya idadi hiyo kufikia wanane, akiwemo mtoto wa miaka saba. Alisema uthibitisho huo unaonesha tena kuwa polio ni tishio kwa watu wote, bila kujali umri, katika maeneo ambayo kinga ya watu imepungua.

Afisa huyo alisema jumla ya watoto milioni 1.96 walio chini ya umri wa miaka mitano walichanjwa katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo iliyofanyika mwezi Agosti.