Umoja wa Afrika waidhinisha ombi la Somalia la kusitisha kuondoa wanajeshi kwa miezi 3
2023-10-06 09:00:00| CRI

Baraza la Amani na Usalama (PSC) la Umoja wa Afrika (AU) limeidhinisha ombi la Somalia la kusitisha kwa miezi mitatu kuwaondoa wanajeshi 3,000 walioko nchini humo.

PSC, pia ilikaribisha ahadi ya nchi zinazochangia askari zikiwemo Kenya, Ethiopia, Burundi, Djibouti na Uganda kushirikiana na Somalia na washirika kupata usaidizi wa kifedha unaohitajika kwa Tume ya Mpito ya AU nchini Somalia (ATMIS).

Nchi hizo tano zinazochangia askari zililiambia Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika kwamba "wanaunga mkono sana usitishaji wa kiufundi" wa kuwaondoa askari hao kwa sababu wanakubaliana na Somalia kwamba nchi inahitaji muda kurekebisha mapungufu kadhaa ya usalama, ikiwa ni pamoja na kukusanya wafanyakazi wa kutosha wa kuchukua majukumu ya usalama.