Jenerali Mkuu wa Kikosi cha Wanajeshi wa Sudan (SAF) Abdel Fattah Al-Burhan Alhamisi alisema jeshi lake litapambana na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) hadi mwisho hata kama wakibakiwa na askari mmoja tu.
Al-Burhan, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Utawala wa Sudan, aliyasema hayo alipokuwa akihutubia Divisheni ya 18 ya Askari wa miguu katika mji wa Kosti Jimboni White Nile. Pia mkuu huyo wa jeshi aliapa kujibu vikali kwa "uhalifu wa RSF" katika kijiji cha Wad Al-Noura Jimboni Gezira, shambulio ambalo liliua zaidi ya raia mia moja.
Wakati huohuo kamati ya upinzani ya Karari, kundi maarufu lisilo la kiserikali, lilitoa taarifa kwenye ukurasa wake wa Facebook likisema takriban raia 22 waliuawa siku ya Alhamisi kutokana na shambulizi la mizinga lililofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kwenye vitongoji kadhaa vya makazi ya mji wa Omdurman, kaskazini mwa Khartoum.
Taarifa hiyo ilisema, kwa mujibu wa taarifa za Hospitali ya Mafunzo ya Al-Nao, raia 22 waliuawa na wengine 45 kujeruhiwa, ikibainisha kuwa idadi ya wahanga wa shambulio hilo katika maeneo mengine bado inahesabiwa.