EAC yazindua mpango wa kuibua uwezo kamili wa biashara za kilimo katika jumuiya hiyo
2023-10-06 08:56:27| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikishirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), zimezindua mpango wa kikanda wenye thamani ya EURO milioni 40 ambao unalenga kuibua uwezo kamili wa wafanyabiashara wa kilimo ndani ya jumuiya hiyo ya kikanda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika Makao Makuu ya EAC mjini Arusha, EAC na EU zilizindua rasmi awamu ya pili ya Mpango wa Kuboresha Ufikiaji Masoko wa EU-EAC (MARKUP II).

Ikitekelezwa na Kituo cha Biashara cha Kimataifa kwa kushirikiana na Sekretarieti ya EAC, MARKUP II itaimarisha biashara ndogo ndogo za EAC kwa kuongeza biashara ya kikanda na kimataifa ikishirikiana kwa karibu na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki, nchi wanachama wa EAC, mashirika ya kusaidia biashara na taasisi za ndani.

Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki amesema mpango wa MARKUP umetoa mchango mkubwa katika uongezaji thamani kupitia uboreshaji wa usindikaji wa kahawa, uhakiki wa ladha na harufu ya kahawa, ufanisi wa rasilimali na uzalishaji wa mzunguko katika sekta ya chai na kahawa za kanda hii.