China yapinga vikali hatua ya Japan kumwaga maji taka yaliyochafuliwa na nyuklia baharini
2023-10-06 08:57:05| CRI

Kampuni ya Nishati ya Umeme ya Tokyo (TEPCO) Alhamisi ilitangaza kuwa imeanza kumwaga maji taka yaliyochafuliwa na nyuklia ya Fukushima kwa awamu ya pili na inapanga kuachia tani 7,800 za maji hayo kwa muda wa siku 17.

Kufuatia hatua hiyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alijibu kwa kusema msimamo wa China juu ya umwagaji huo ni thabiti na uko wazi kwamba inapinga vikali hatua hii ya upande mmoja ya Japan.

Aidha msemaji huyo alisisitiza tena kuwa bahari ni mali ya binadamu wote. Serikali ya Japan inahitaji kujibu wasiwasi wote wa jumuiya ya kimataifa, kuwa na mawasiliano kamili na ya dhati na nchi jirani, na kutupa maji taka ya nyuklia kwa njia sahihi.

Amebainisha kuwa jumuiya ya kimataifa inahitaji kushinikiza kuwepo kwa mpango wa ufuatiliaji wa kimataifa ambao utaendelea kuwa na ufanisi kwa muda mrefu na kuhakikisha kuwa nchi jirani za Japani na wadau wengine wanaweza kushiriki kwa kiasi kikubwa katika mpangilio huo.