IGAD yaonya kuhusu ukosefu wa utulivu wa kisiasa na msimamo mkali katika kanda ya Pembe ya Afrika
2023-10-09 08:30:38| CRI

Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) limesema, kuongezeka kwa makundi yenye msimamo mkali katika baadhi ya nchi za Pembe ya Afrika kunaweza kuzorotesha juhudi za kukabiliana na ukosefu wa usalama, uharamia na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Mwakilishi maalum wa IGAD kuhusu Bahari Nyekundu, Ghuba ya Aden na Somalia, Mohammed Ali Guyo amesema mjini Naivasha, nchini Kenya, kuwa hali katika eneo hilo imechochewa na ukame wa hivi karibuni uliowafanya maelfu ya watu kukimbia makazi yao. Amesema kanda hiyo imeshuhudia kuibuka kwa ugaidi, uharamia, na wizi wa kutumia silaha, pamoja na utekaji nyara baharini, na kwamba ukosefu wa operesheni za usalama kati ya nchi wanachama zimefanya hali hiyo kuwa mbaya zaidi.

Bw. Guyo amesema hayo baada ya kikosi kazi kilichoanzishwa na IGAD kwa lengo la kutambua changamoto na fursa katika Ghuba ya Aden na Bahari Nyekundu kuwasilisha ripoti yake kwa nchi nane wanachama wa Shirika hilo.