Afrika kuwa na sauti zaidi kwenye IMF kufuatia kupata kiti katika bodi yake ya utendaji
2023-10-09 10:30:14| cri

Afrika inatarajiwa kuwa na sauti zaidi katika shirika la fedha la kimataifa IMF baada ya kupata kiti cha tatu kwenye bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo. Mkurugenzi wa IMF Bibi Kristalina Georgieva ametoa habari hiyo kabla ya mikutano ya wiki ijayo ya IMF na Benki ya Dunia huko Marrakesh, Morocco itakayofanyika kwa mara ya kwanza barani humo tangu 1973. Bodi kuu ya IMF, ambayo inaongozwa na mwenyekiti wake, Bibi Georgieva, ina jukumu la kuendesha taasisi hiyo yenye makao yake makuu Washington ambayo kwa sasa ina wakurugenzi 24.

Marekani, ikiwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, ina sehemu kubwa zaidi ya kura, ikifuatiwa na mataifa yenye nguvu kiuchumi Japan, China na Ulaya magharibi, mbele ya kanda nyingine na nchi zinazoendelea.

Bibi Georgieva amesema hiyo ni habari njema kwa Afrika, kwani sasa wanajipanga kuwa na mwakilishi wa tatu wa Afrika kutoka eneo la kusini mwa Sahara kwenye bodi ya utendaji ya shirika hilo, hii ina maana kubwa kwamba Afrika itakuwa na sauti zaidi. Benki ya Dunia pia imetangaza kuwa itatenga kiti cha tatu cha nchi ya Afrika katika bodi yake ya wakurugenzi, uamuzi utakaofanywa rasmi katika mikutano hiyo inayofanyika Oktoba 9-15 mjini Marrakesh.