Zaidi ya watu laki moja wakosa makazi kufuatia mafuriko ya ghafla kusini magharibi mwa Somalia
2023-10-09 08:31:11| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, mafuriko ya ghafla yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha jumatano yamesababisha watu 107,000 katika wilaya ya Baidoa, kusini magharibi mwa Somalia kukosa makazi.

Ofisi hiyo imesema jana kuwa, nyumba kadhaa ziliharibiwa na mafuriko hayo, ikiwemo mahema yanayohifadhi zaidi ya wakimbizi wa ndani 86,700 katika kambi 136 wilayani Baidoa.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, watu milioni 1.2 na hekta milioni 1.5 za mashamba ziko hatarini kutokana na mafuriko nchini Somalia. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema kuwa linahitaji dola za kimarekani milioni 11.8 ili kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kutambua maeneo yaliyo hatarini kukabiliwa na mafuriko kabla ya mvua za El-Nino kuanza nchini Somalia.