Mambo matatu yatajwa sababu za kuongezeka kwa watalii Tanzania
2023-10-10 10:06:52| cri

Wanyamapori, fukwe za bahari na Mlima Kilimanjaro ni vivutio vinavyotajwa kuchangia ongezeko la idadi ya watalii nchini Tanzania.

Katika kipindi cha Januari hadi Agosti, 2023 idadi ya watalii nchini humo imeongezeka na kufikia 1,131,286 ikilinganishwa na idadi ya watalii 900,182 walioingia kipindi kama hicho mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 25.7.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk. Daniel Masolwa amesema kati ya watalii walioingia Tanzania mwaka huu, watalii 236,047 walioingia kupitia Zanzibar ni sawa na asilimia 31.1 ya watalii wote.

Aidha alisema katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2023, pia walipokea watalii kutoka Afrika ambapo idadi kubwa ilitoka Kenya watalii 128,753, Burundi 69,505, Zambia 38,398 na Rwanda 37,269.