Iran na Sudan zatangaza kurejesha rasmi uhusiano wa kidiplomasia
2023-10-10 10:07:35| cri

Jana Oktoba 9, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitoa taarifa ya pamoja ya Iran na Sudan ikisema kwamba baada ya miezi kadhaa ya mikutano na mawasiliano kati ya maafisa waandamizi wa Iran na Sudan, pande hizo mbili zimeamua kurejesha uhusiano wa kidiplomasia ili kuendeleza maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa serikali hizo mbili zilikubaliana kuendeleza uhusiano wa kirafiki unaozingatia kuheshimiana kwa uhuru, usawa, kulinda maslahi ya pamoja na kuishi pamoja kwa amani. Pande hizo mbili zimekubaliana kupanua ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali kama vile kutimiza maslahi ya pamoja na kuhakikisha usalama na utulivu wa kikanda. Pia zilikubaliana kuchukua hatua zinazohitajika kufungua balozi za kila upande katika siku za usoni na kuweka mipango ya ziara za kutembeleana ili kutafuta njia za kupanua ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.