Rais Xi akutana na ujumbe wa bunge la Marekani
2023-10-10 08:37:14| CRI

Rais Xi Jinping wa China amekutana na ujumbe wa bunge la Marekani ukiongozwa na kiongozi wa wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer leo Jumatatu mjini Beijing.

Rais Xi alisema uhusiano kati ya China na Marekani ni uhusiano muhimu zaidi wa pande mbili duniani, na jinsi China na Marekani zinavyopatana ndio itaamua mustakabali na hatma ya binadamu. Ushindani na makabiliano haviendani na mwelekeo wa zama za leo, na pia haviwezi kutatua matatizo ya nchi zenyewe na changamoto zinazoikabili dunia. China siku zote imekuwa ikiamini kwamba maslahi ya pamoja ya China na Marekani ni makubwa kuliko tofauti zao, na kwamba mafanikio ya China na Marekani ni fursa na sio changamoto kwa upande mwingine.

Naye Bw. Chuck Schumer alisema kwamba maendeleo thabiti ya uhusiano kati ya Marekani na China sio tu ni muhimu kwa Marekani na China, bali pia yanahusiana na amani na maendeleo ya dunia. Maendeleo na ustawi wa China yananufaisha watu wa Marekani. Marekani haitafuti mgogoro na China wala haitaki kutengana na China, bali inapenda kuimarisha mazungumzo na mawasiliano na China kwa moyo wa dhati na kuheshimiana, kushughulikia na kudhibiti ipasavyo tofauti kati ya nchi hizo mbili na kuhimiza maendeleo thabiti ya uhusiano wa Marekani na China.