Watoto milioni 19 nchini Sudan hawaendi shuleni wakati mapigano yakiendelea nchini humo
2023-10-10 08:37:40| CRI

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) na Shirika la Save the Children yamekadiria kuwa, watoto milioni 19 nchini Sudan hawaendi shule wakati mapigano ya kijeshi nchini humo yakiingia katika mwezi wa sita wiki ijayo.

Katika taarifa yao ya pamoja kwa vyombo vya habari, Mashirika hayo yamesema, kati ya watoto hao, milioni 6.5 wanashindwa kwenda shule kutokana na mapigano makali na ukosefu wa usalama katika mikoa yao, huku shule karibu 10,400 zikifungwa katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano.

Mashirika hayo yamesema, hata kabla ya vita vilivyoanza April 15 mwaka huu, karibu watoto milioni 7 walikuwa nje ya shule, na kuonya kuwa, kama vita hiyo ikiendelea, hakuna mtoto nchini Sudan atakayeweza kurudi shule katika miezi ijayo, na hivyo kuwaweka katika hatari za muda mrefu, ikiwemo kuwa wakimbizi wa ndani, kuandikishwa katika makundi ya silaha na uhalifu wa kingono.