Benki ya Dunia yafadhili miradi mitatu kuongeza ufanisi katika utoaji elimu
2023-10-11 10:28:23| cri

Benki ya Dunia (WB) imefadhili miradi mitatu katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ambayo imewezesha kujenga vituo vya umahiri katika utoaji wa mafunzo ya elimu ya juu.

Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Maulilio Kipanyula wakati akizungumza mara baada ya wageni kutoka benki ya dunia kutembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kujionea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na benki hiyo. Amesema uwepo wa miradi hiyo umefanya uwezo wa taasisi kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuweka mifumo ya kiutendaji na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA katika kuboresha mitandao ya mawasiliano sambamba na maeneo ya kufundishia na kufanyia utafiti kwa upande wa maabara.

Ameongeza kuwa Benki ya Dunia inafadhiili miradi mitatu katika taasisi hiyo huku miwili ikiwa ni vituo vya umahiri Afrika vinavyolenga katika utoaji wa mafunzo elimu ya juu katika ngazi ya uzamili na uzamivu ambavyo ni CREATES -FNS, na WISE -Futures na miradi hiyo miwili ilianza mwaka 2017 na inaishia Desemba mwaka huu.