Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” la China lasaidia Afrika kupata maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali
2023-10-11 14:52:04| CRI

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Humphrey Moshi amesema Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” la China limesaidia Afrika kupata maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali.

Prof. Moshi amesema hayo alipofanyiwa mahojiano na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG), ambapo amesema maendeleo hayo yamepatikana barani Afrika katika pande tatu.

Kwanza, Tanzania na nchi nyingi za Afrika zimepata maendeleo ya kasi ya kiuchumi, kwani kutokana na pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China imejenga barabara, vifaa vya uzalishaji wa umeme, uhifadhi wa maji pamoja na miundombinu mingine barani Afrika, na kuleta maendeleo ya kasi ya uchumi ya sehemu hizo.

Pili, kasi ya kupunguza umaskini barani Afrika imeongezeka. Amesema Afrika ni bara lenye idadi kubwa zaidi ya watu maskini duniani, na zaidi ya watu milioni 400 bado wanaishi katika umaskini, na kutokana na pendekezo hilo, idadi ya watu maskini barani Afrika inapungua.

Mwisho, amesema sekta ya viwanda inaendelea kukua kwa kasi, na kwamba hivi sasa uchumi wa Afrika hautegemei tena kilimo tu. Kutokana na Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, viwanda vya Afrika pia vinaendelezwa, na mchakato wa viwanda utasaidia nchi za Afrika kuinua hadhi zao.

Aidha Prof. Moshi amesema anatumai kuwa ushirikiano kati ya Afrika na China utaendelea.