Tanzania yakaribia kugundua mafuta wakati imekamilisha kupata data za 2D seismic
2023-10-11 23:12:43| cri

Tanzania imekamilisha upatikanaji wa data za 2D seismic katika Bonde la Eyasi Wembere, hatua ambayo ni muhimu katika azma ya nchi hiyo ya kugundua mafuta na gesi asilia. Mradi huo uliogharimu Sh8 bilioni, unaendeshwa katika maeneo ya ndani ya wilaya sita katika mikoa mitano ambayo ni Singida, Arusha, Tabora, Shinyanga na Simiyu.

Bonde hilo linaaminika kwamba lina uwezo wa kuwa na rasilimali muhimu za mafuta na gesi, kutokana na mfanano wake wa kijiolojia na mabonde mengine yanayozalisha mafuta katika eneo hilo, kama vile mabonde ya Albertine na Turkana nchini Uganda na Kenya, mtawalia.

Akizungumza na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mtaalamu wa Jiofizikia kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Meneja wa Mradi Bw Sindi Maduhu, alieleza kuwa upatikanaji wa data za 2D seismic utasaidia nchi hiyo kutambua maeneo yenye dalili za uwezekano wa kuwepo kwa mafuta na gesi asilia.