Mjumbe maalumu wa China katika Mashariki ya Kati azungumza na ofisa wa Misri anayeshughulikia masuala ya Palestina
2023-10-11 11:07:46| cri

Mjumbe maalumu wa serikali ya China anayeshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati Bw. Zhai Jun jana aliwasiliana kwa njia ya simu na waziri msaidizi wa masuala ya Palestina katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, Osama Khedr, kuhusu hali ya Palestina na Israel.

Bw. Zhai amesema kuwa China ina wasiwasi mkubwa kuhusu kushamiri kwa mivutano na ghasia kati ya Palestina na Israel, na inasikitishwa kuona idadi kubwa ya vifo vya raia vilivyosababishwa na vita hivyo. China inapinga na kulaani vitendo vinavyodhuru raia na kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja. Mgogoro wa Palestina na Israel umekuwa ukiendelea kwa mzunguko, na kiini chake bado ni kushindwa kutatuliwa kwa haki kwa suala la Palestina. Ufumbuzi wa msingi uko katika utekelezaji wa “suluhu ya nchi mbili”.

China inapenda kudumisha mawasiliano na uratibu na Misri, kuhimiza pande mbili za mgogoro kusitisha mapigano na kukomesha ghasia haraka iwezekanavyo.

Osama ameshukuru msimamo wa muda mrefu na wa haki wa China kuhusu suala la Palestina, na kusisitiza kuwa suala la Palestina linapaswa kutatuliwa kwa haki kwa msingi wa “suluhu ya nchi mbili” kwa mujibu wa maazimio husika ya Umoja wa Mataifa. Misri inatarajia kushirikiana na China katika kujitahidi kutuliza hali kati ya nchi hizo mbili.