IGAD yatoa taarifa ya pamoja kuhusu kuimarisha usalama katika kanda ya Ghuba ya Aden
2023-10-11 08:44:55| CRI

Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) limetoa taarifa ya pamoja inayolenga kuboresha amani na usalama katika Ghuba ya Aden na Bahari Nyekundu.

Makubaliano ya Mpango Kazi wa Kikanda (RPA) na Msimamo wa Pamoja yaliyofikiwa na nchi nane wanachama wa IGAD yatasaidia kukabiliana na matishio ya usalama kama uharamia, utekaji nyara na kuibuka kwa makundi ya msimamo mkali katika kanda hiyo inayotumika kwa biashara ya baharini kwa zaidi ya asilimia 10.

Katika taarifa hiyo ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano wa siku tatu uliofanyika katika mji wa Naivasha nchini Kenya, IGAD imesema utekelezaji wa makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kutimiza utulivu wa kudumu.

Mjumbe maalum wa IGAD kuhusu Bahari Nyekundu, Ghuba ya Aden na Somalia, Mohamed Ali Guyo amesema, mapendekezo hayo yatasaidia kukabilian na matishio ya usalama katika Ghuba ya Aden na Bahari Nyekundu.