Pendekezo la "Ukanda Mmoja na Njia Moja" lapata mafanikio mengi
2023-10-11 08:40:34| cri

Miaka 10 iliyopita wakati Rais Xi Jinping anatangaza kuanzishwa kwa pendekezo la “ukanda mmoja, njia moja” (Belt and Road Initiative) si watu wengi waliokuwa wanajua kuwa pendekezo hili lingekuwa ni mkombozi wa nchi nyingi dunia, hasa zile zilizotambua kuwa kukosekana kwa miundo mbinu katika nchi zao ndio kikwazo kikubwa cha maendeleo. Lakini pia si wataalamu wengi waliojua kuwa pendekezo hili litakuwa jukwaa la nchi za magharibi kuipaka matope China.

Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China leo Oktoba 10 imetoa waraka mweupe (White Paper) kuhusu Kujenga Kwa Pamoja Ukanda Mmoja, Njia Moja: Kazi Muhimu kwenye Kujenga Jumuiya ya Binadamu yenye Hatma ya Pamoja.

Waraka huo umefafanua kwa kina kuhusu historia, ruwaza, mipango, mafanikio na umuhimu wa ujenzi wa pamoja wa Ukanda Mmoja, Njia Moja kwa dunia nzima. Waraka huo umefahamisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka kumi iliyopita tangu pendekezo la Ukanda Moja, Njia Moja litolewe, na pia umesisitiza dhamira na hatua za China kusukuma mbele maendeleo yenye ubora wa hali ya juu ya Ukanda Moja, Njia Moja, na kushirikiana na mataifa mengine katika kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja.

Katika kipindi cha miaka mitatu au minne iliyopita, kama ulikuwa unafuatilia habari zinazoandikwa na vyombo vya habari vya Afrika na nchi za dunia ya tatu kuhusu pendekezo la ukanda mmoja, basi unaweza kutambua kuwa maendeleo makubwa ya sekta ya miundombinu katika nchi hizo, yametokana na mchango mkubwa uliotokana na utekelezaji wa miradi iliyogharamiwa chini ya mpango wa pendekezo la “ukanda mmoja, njia moja”. Lakini kama ulisoma habari katika vyombo vya habari vya nchi za magharibi, basi habari nyingi zilikuwa ni hasi na kulihusisha pendekezo hilo na kinachoitwa “mtego wa madeni”.

Kikubwa kilichotajwa wakati pendekezo hili linatangazwa, ni kuwa moja ya changamoto kubwa za maendeleo duniani, ni swala la muunganiko (interconnectivity). Na bila kutatuliwa kwa suala hili, kufikia maendeleo litakuwa ni jambo gumu sana. Ndio maana tumeona miradi iliyojengwa chini ya pendekezo hilo kama ule wa Reli ya SGR ya Mombasa - Nairobi Kenya, Reli ya Kaduna- Abuja ya Nigeria, Reli ya Addis Ababa – Djibouti, na miradi mingine mingi ya barabara na viwanja vya ndege, na miradi mingine mingi ilivyopunguza tatizo la usafiri na usafirishaji katika nchi za Afrika na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi hizo.

Waingereza wanasema seeing is believing, kwa watu wa Afrika, pendekezo la “Ukanda mmoja, njia moja” si jambo la kufikirika, bali ni jambo halisi ambalo matokeo yake yanagusa moja kwa moja kwa njia chanya maisha ya watu. Si reli wala barabara tu, kuna miradi ya umeme, maji, miundombinu ya huduma za afya na mingine mingi ambayo inaonekana.

Vyombo vya habari vyenye hila vya nchi za magharibi vilikuwa na lugha mbalimbali za kejeli kuhusu pendekezo hilo, wakiamini kuwa halitafika popote. Ukweli ni kuwa huu ni mwaka wa 10, pendekezo hilo bado lipo na linaendelea kwa nguvu. Uzuri ni kwamba na matarajio kuhusu pendekezo hilo, kwa wale wenye mahitaji na hata kwa China yenyewe yanazidi kuongezeka. Hivi karibuni mchambuzi mmoja wa mambo ya hisa wa mji wa Shanghai, aliiambia televisheni CNBC ya Canada kuwa China bado iko imara kwenye kuhimiza utekelezaji wa pendekezo hilo.

Lakini ni kweli pia kuwa Seeing is believing. Tukiangalia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, nchi za magharibi zimejitokeza na ahadi kubwa kubwa kuhusu kuja na pendekezo lililo bora zaidi kwa nchi zenye mahitaji. Marekani ilitangaza pendekezo lake (B3W initiative), Uingereza ilitangaza pendekezo lake na kundi la G7 pia limekuja na mpango wake (PGII Partnership for Global Infrastructure Investment). Hadi sasa hakuna chochote kikubwa kilichoonekana, kinachoweza kukaribia japo kwa nusu ya kile kilichofanyika chini ya pendekezo la “ukanda mmoja, Njia moja”.

Mara nyingi China imekuwa inasema ni jambo jema kwa nchi mbalimbali kuhimiza maendeleo ya nchi za dunia ya tatu, na wala sio kufanya ushindani. Lakini ni hadi pale watu wa nchi hizo watakapoweza kuona kwa macho yao, kile kinachosemwa na nchi za magharibi, ndipo watakuja kuamini.