Licha ya changamoto zinazowakabili walimu wanawake bado wanaendelea kulisukuma mbele gurumu la elimu
2023-10-13 08:00:30| CRI

Walimu ndio kiini cha elimu, bila ya wao kusingekuwa na wataalamu mbalimbali ambao sasa tunajivunia nao. Kazi kubwa wanayoifanya inastahili kupongezwa sana, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakiwaachia mzigo mkubwa na kama haitoshi hata kuwatupia lawama walimu hawa. Hata kwa upande wa maslahi yao pia wamekuwa wakisahauliwa, ambapo katika sehemu nyingi duniani sekta hii ya elimu na walimu kwa jumla ndio wanaopokea mshahara mdogo kabisa licha ya kwamba wanafanya kazi kubwa ya kuibua vipaji vya watu mbalimbali.

Ikiwa dunia kila mwaka inasherehekea siku ya walimu duniani yaani tarehe 5 Oktoba ambayo ni wiki iliyopita, tunapaswa kukaa chini na kutafakari ili tujue tunakosea wapi na wapi tunatakiwa turekebishe ili kuwaondoa unyonge walimu hawa ambao wanavuja jasho ili kuhakikisha maslahi ya watoto wetu na mustakabali wao unakuwa mzuri. Hivyo leo katika kipindi cha Ukumbi Wanawake leo tutaangalia changamoto zinazowakabili walimu wanawake na juu ya hivyo bado wanaendelea kulisukuma mbele gurumu la elimu.