Ripoti kuhusu uwekezaji na mikopo katika nchi za Afrika yaonesha China imeongeza uwekezaji wake na kuna athari chanya kwenye mikopo
2023-10-12 14:43:16| cri

Idara ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa ya Taasisi ya Uchumi wa Muundo Mpya ya Chuo Kikuu cha Beijing leo imezindua ripoti kuhusu uwekezaji na mikopo katika nchi za Afrika.

Ripoti hiyo iliyopewa jina la “Uchunguzi juu ya Ufanisi wa Ufadhili wa China katika Afrika”, inaonesha kuwaufadhili katika kipindi cha mwaka 2006, hasa baada ya msukosuko wa fedha wa mwaka 2008 umeongezeka kwa kasi na kiasi kikubwa ambapo katika miongo miwili iliyopita kutoka mwaka 2000 hadi 2020, China kwa ujumla imetoa ufadhili wa dola za Kimarekani bilioni 160 kwa nchi za Afrika ambapo mingi 90% imekwenda kwa nchi zenye mapato ya chini na kati.

Kwa mujibu wa takwimu za ripoti hiyo, athari chanya za mikopo ya China kwa ukuaji wa uchumi wa Afrika zimekua kutoka asilimia 0.176 hadi 0.300 ikiashiria kwamba ongezeko la mikopo la asilimia 1 limechangia ukuaji wa uchumi wa Afrika angalau kwa asilimia 0.176.

Akiwa miongoni mwa jopo la wataalamu waliojadili ripoti hiyo balozi wa Zambia nchini China Ivan Zyuulu amesema China imefanya mambo makubwa katika kusaidia Afrika hata hivyo ameshauri kwamba uwezkezaji pia uongezwe zaidi kwenye sekta ya kilimo.

 “Kuna matokeo madogo sana kwenye uwekezaji wa sekta ya kilimo, na bahati nzuri kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi za Afrika, ndio maana tunataka kuona matokeo katika upande huo. Hata kama tunawekeza zaidi kwenye miundo mbinu, lakini tungependa kuona inasaidia bidhaa za kilimo kuhama na kuingia maeneo yenye mahitaji zaidi yenye walaji. Hivyo hili ndilo eneo ambalo linahitaji uungwaji mkono zaidi kutoka China, ili kuona sekta ya kilimo inaendana na uwekezaji wetu.” balozi Zyuulu alisema.

Kwa upande wake balozi wa Malawi nchini China amesema katika miaka yote hiyo hakuna nchi ya magharibi iliyojikita katika uwekezaji wa miundo mbinu isipokuwa China, na hii ni miradi ghali zaidi ikilinganishwa na ile inayofadhiliwa na nchi za magharibi ambayo hata nchi za Afrika pia zinashindwa kuitekeleza wao wenyewe bila msaada wa wafadhili. Hata hivyo amebainisha kuwa tatizo kubwa lipo kwenye muundo wa uwekezaji ambao hadi sasa nchi za Afrika zinafuata ule wa Benki ya Dunia na IMF na sio wa China.

 “Kutokana na uzoefu wangu kwenye muudo wa miradi inayowekezwa na China, ni kwamba ningeshauri sasa tuondoke kwenye masuala ambayo IMF na Benki ya Dunia wametufanya tuyafanye kutokana na muundo wao ambayo naamini ni makosa, na kwa njia hiyo pia tutaimarisha ushirikiano wetu na China kwasababu ushirikiano huu ni wa kweli na wa uaminifu”. balozi wa Malawi alisema.