Ndege ya KQ kutoka Nairobi hadi London yaelekezwa kutua uwanja wa ndege wa Stansted badala ya Heathrow
2023-10-13 10:03:26| cri

Polisi nchini Uingereza wamethibitisha kuwa ndege ya shirika la ndege la Kenya KQ kutoka Nairobi ilielekezwa kutua Uwanja wa Ndege wa Stansted badala ya uwanja wa ndege wa Heathrow London siku ya Alhamisi, Oktoba 12, alasiri.

Ndege hiyo KQ100 ilielekezwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Stansted, ambao umeteuliwa kwa matukio ya usalama. Sababu ya kutua huko inasemekana kuwa ni tishio la usalama, na vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa vikosi vya mabomu vilionekana kukimbilia eneo la tukio.

Katika taarifa, KQ ilithibitisha kuwa ndege yake ya KQ100 kutoka Nairobi hadi Heathrow London "ilipokea tahadhari ya tishio la usalama".

Ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliondoka Nairobi saa 3:18 asubuhi, baada ya kuchelewa kwa dakika 13.

Tukio hilo linakuja siku moja baada ya kutangazwa kuwa Mfalme wa Uingereza Charles III na mkewe Malkia Camilla watafanya ziara ya kitaifa ya siku nne nchini Kenya mwishoni mwa mwezi huu.