Tanzania kupambana mabadiliko tabia nchi
2023-10-13 23:33:50| cri

Serikali ya Tanzania imesaini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano na Shirika la NORAD la nchini Norway kwa ajili ya tafiti za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi, kwa ufadhili unaogharimu Sh bilioni 9.

Makubaliano hayo yamefikiwa Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dk Amos Nungu pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Watu kutoka Balozi za Norway na Sweden Lisa Sivertsen, na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk Selemani Jafo akiwa na Balozi wa Norway nchini Tonne Tines na Balozi wa Sweden Charlotta.

Akizungumza Jafo amesema makubaliano hayo yamefikiwa baada ya mkataba uliosainiwa Septemba mwaka huu wa ushirikiano na Norway wa program ya miaka mitano ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi inayotekelezwa na Costech.

Amesema fedha hizo zilizotolewa na Norway zitatumika na watafiti nchini humo kwa ajili ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kuangalia namna ya kupunguza athari. Amewaomba watafiti kujikita kufanya tafiti zenye kuleta tija Kwa matatizo yanayoikumba jamii, kwamba kama ni eneo la kilimo hali iweje na pia miundombinu ujenzi wake uwe wa namna gani.