Kampuni 16 za Tanzania ‘kuvamia’ soko la China
2023-10-13 10:05:55| cri

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) Profesa Ulingeta Mbamba amesema jumla ya kampuni 16 yamejisajili kwenda kutangaza bidhaa zao kwenye maonesho ya sita ya kimataifa nchini China (CIIE).

Maonesho hayo yaliyoanzishwa tangu mwaka 2018, hadi sasa mataifa 51 yameshiriki kwa kuonesha bidhaa zao, ambapo mwaka huu maonesho hayo yanatarajiwa kuanza Novemba mosi, katika mji wa Shanghai.

Akizungumza Dar es Salaam jana Oktoba 12 kwenye hafla ya kuwaaga wafanyabiashara hao katika Ofisi za Ubalozi wa China, Profesa Ulingeta amesema bado wanaendelea kusajili wafanyabiashara wenye nia ya kushiriki maonesho hayo. Amesema ni muhimu kwa Watanzania kulitumia soko hilo na kufungua fursa za kutangaza bidhaa zao zinazozalishwa nchini na kulifikia soko la China na dunia kwenye bidhaa za kilimo, madini na utalii.

Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema kadri miaka inavyokwenda maonesho hayo yameendelea kuwa bora na ya mfano kwa kuwa yanakusanya bidhaa kutoka mataifa mbalimbali. Ameongeza kuwa China bado inatoa kipaumbele kwa mataifa ya Afrika kupeleka bidhaa zake katika soko hilo.