Msomi wa Nigeria: “Ukanda Mmoja, Njia Moja” wasukuma mbele uendelezaji wa viwanda barani Afrika
2023-10-16 08:35:07| CRI

Katika muongo uliopita, matokeo yaliyopatikana kwenye ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” yamenufaisha nchi nyingi za Afrika, na kutoa msukumo wa maendeleo kwa nchi zinazoshiriki kwenye ujenzi huo. Mtaalamu wa masuala ya kimataifa wa Nigeria Dkt. Michael Ehizuelen alipohojiwa hivi karibuni na Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG, amesema matokeo ya ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” yanaonekana mahali popote barani Afrika, ambako miundombinu imeboreshwa kidhahiri, na ujenzi wa maeneo ya viwanda unaendelea hatua kwa hatua. “Ukanda Mmoja, Njia Moja” umesukuma mbele kwa nguvu mchakato wa kuendeleza sekta ya viwanda barani Afrika.

Dkt. Ehizuelen amesema, katika ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”,  miradi mingi ya miundombinu imetekelezwa barani Afrika, ikiwemo reli ya Addis Ababa-Djibouti, reli ya Mombasa-Nairobi nchini Kenya, reli ya Abuja-Kaduni na reli ya Lagos-Ibadan nchini Nigeria, ambayo imelisaidia bara la Afrika kutimiza muunganiko wa ndani. Amesema, maendeleo hayo pia yatazisaidia nchi za Afrika kuvutia zaidi uwekezaji wa kigeni, kukuza biashara ya nje, na hatimaye kupunguza umaskini.

Dkt. Ehizuelen amesema, katika mchakato wa kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China na nchi za Afrika zimejitahidi kusukuma mbele ujenzi wa maeneo ya viwanda. Maboresho ya mitandao ya reli yakihimizana na maendeleo ya maeneo ya viwanda, yatatoa mchango chanya katika mchakato wa kuendeleza sekta ya viwanda ya Afrika, na vilevile kuongeza uhai kwenye ukuaji wa uchumi wa Afrika. Kupitia ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China imeisaidia Afrika kuinua hatua kwa hatua uwezo na kiwango chake cha kujiunganisha kwenye uchumi wa dunia. “Ukanda Mmoja, Njia Moja umefungua njia mpya kwa ushirikiano wa kiwango cha juu zaidi kati ya Afrika na China”, amesema Dkt. Ehizuelen.