Tanzania yazitaka Benki ya Dunia na IMF kutambulisha Kiswahili kama lugha ya kikazi
2023-10-16 09:04:33| CRI

Tanzania imetoa ombi kwa Kundi la Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kutambulisha Kiswahili kama lugha ya kikazi.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango ya nchi hiyo imesema, ombi hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar anayeshughulika na Fedha na Mipango Bi. Saada Mkuya wakati akihutubia mkutano wa mwaka 2023 wa Benki ya Dunia na IMF uliofanyika Marrakech nchini Morocco. Bi. Mkuya amesema Kiswahili tayari kinatumika kama lugha rasmi katika mashirika kadhaa ya kikanda, ikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika, na Umoja wa Afrika.

Ameongeza kuwa, Kiswahili ni moja kati ya lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi duniani, kikiwa na zaidi ya watu milioni 200 wanaozungumza lugha hiyo.