Tanzania yataka kutangaza michuano ya AFCON 2023 kwa Kiswahili
2023-10-17 09:02:53| CRI

Mamlaka ya Tanzania imesema imewasilisha ombi kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) la kutangaza kwa lugha ya Kiswahili Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2023.

Akiongea jana alipofanya ziara kwenye ofisi za Baraza la Kiswahili Tanzania BAKITA, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Bw. Damas Ndumbaro amesema kukiwa na zaidi ya watu milioni 200 wanaozungumza Kiswahili duniani, AFCON 2023 litakuwa jukwaa bora la kukuza lugha hiyo. Amesema kama CAF itaridhia ombi la Tanzania, itatuma watangazaji wake kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania kwenda nchini Cote d’Ivoire.

Fainali za kombe hilo zitakazojumuisha timu 24 zilizotakiwa kufanyika mwaka huu, zitafanyika kati ya Januari 13 na Februari 11 mwaka kesho nchini Cote d’Ivoire baada kucheleweshwa kwa muda.

Waziri Ndumbaro amesema fainali hizo zitatumika kama maandalizi ya kutangaza kombe la AFCON 2027 litakaloandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.