Mwanariadha wa mbio za marathoni Titus Ekiru afungiwa kwa miaka 10 kutokana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli
2023-10-17 23:31:18| cri

Shirikisho la Riadha Duniani limeendelea kukaza kamba kwa watumiaji dawa za kusisimua misuli baada ya kumfungia mwanariadha wa Kenya Titus Ekiru kwa miaka 10 kwa makosa mbalimbali ya matumizi ya dawa hizo.

Ekiru, ambaye hatakuwa tena mwanariadha wa sita kwa kasi zaidi katika historia ya mbio za marathoni, anaweza pia kuhesabu kuwa kibarua chake kwenye riadha kimeota mbawa baada ya chombo cha kusimamia maadili ya wanariadha duniani (AIU) kutoa uamuzi huo Jumatatu.

Ekiru, ambaye kasi yake kubwa kwenye riadha ilikuwa saa mbili, dakika mbili, sekunde 57 alisimamishwa kwa muda na AIU tangu Julai mwaka huu.

AIU ilifichua kuwa Ekiru alishirikiana na daktari wa ngazi ya juu katika hospitali moja nchini Kenya, ambapo chombo hicho tangu wakati huo kilimpeleka daktari huyo kwa Wakala wa Kupambana na Dawa za Kulevya Kenya (ADAK) ili kufunguliwa mashtaka. Ekiru ambaye matokeo yake ya tangu tarehe 16 Mei,2021 yamefutiliwa mbali katika rekodi za Riadha za Dunia, na ambaye atatumikia marufuku ya muongo mmoja nje ya riadha kuanzia Juni 28, 2022, alipatikana na hatia ya Kuwepo kwa Dawa Zilizopigwa Marufuku (Triamcinolone Acetonide na metabolite; Pethidine na metabolite) na kwa kufanya udanganyifu.