China yatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono maendeleo ya Afrika
2023-10-17 08:41:04| CRI

Naibu mjumbe wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Dai Bing, amesema kuunga mkono maendeleo ya Afrika ni jukumu la pamoja la jumuiya ya kimataifa.

Akiongea jana kwenye majadiliano ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo na amani ya Afrika Balozi Dai amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuelewa hali halisi na mahitaji maalumu ya nchi za Afrika, kuheshimu nchi za Afrika zichague njia ya maendeleo inayolingana na hali yao halisi, na kutoa misaada zaidi inayohitajika.

Amesisitiza kuunga mkono amani na utulivu wa Afrika, kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto ya kifedha katika maendeleo yao, na kuweka utaratibu wa kimataifa wenye haki na usawa, kutekeleza kivitendo mfumo wa pande nyingi, kupinga ukoloni na umwamba wa aina yote, kupinga vikwazo haramu vya upande mmoja dhidi ya nchi kadhaa za Afrika, kupanua uwakilishi na sauti ya nchi za Afrika katika mambo ya kimataifa na usimamizi wa dunia, na kuzisaidia nchi za Afrika kuimarisha ujenzi wa uwezo.