UM: Watu karibu 4,000 wauawa huku mamia ya maelfu ya watu wakikimbia mapigano nchini Sudan
2023-10-18 09:13:20| CRI

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema tangu mapigano yaibuke nchini Sudan Aprili 15, watu takriban elfu nne wameuawa na wengine maelfu wamejeruhiwa huku wafanyakazi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wakisema mapigano hayo pia yamesababisha maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani za Sudan Kusini na Chad.

Bw. Dujarric ameongeza kuwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR na washirika wake, wametoa vifaa vya msingi vya msaada kwa familia za wakimbizi kaskazini na magharibi mwa Darfur, na pia Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa wito kwa pande mbalimbali za mgogoro huo kuhakikisha ulinzi wa raia na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu katika maeneo inapohitajika.