Rais Xi Jinping wa China na mkewe waandaa tafrija kuwakaribisha wageni wanaohudhuria mkutano wa kilele wa Ukanda Mmoja, Njia Moja
2023-10-18 08:45:22| CRI

Rais Xi Jinping wa China na mke wake Peng Liyuan jana usiku waliandaa tafrija kwenye Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, kuwakaribisha wageni wa kimataifa waliowasili China kuhudhuria mkutano wa Baraza la Tatu la Ushirikiano wa Kimataifa la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”.

Akiongea kwenye tafrija hiyo, Rais Xi amebainisha kuwa katika miaka 10 tangu alipotoa pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, China imeshirikiana na washirika wake, wakieneza moyo wa Njia ya Hariri unaosisitiza uwazi, ushirikishi, kufundishana na kunufaishana, katika kuchangia mafungamano na muunganiko wa kimataifa, kuweka jukwaa la ushirikiano wa kiuchumi, na kutoa msukumo kwa ukuaji wa uchumi wa dunia.

Rais Xi amesisitiza kuwa kama wataendelea kushikilia lengo la ushirikiano na jukumu la kuleta maendeleo, ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” hakika utafungua mustakbali mzuri zaidi wa binadamu kwa juhudi za pamoja.