Rais Xi Jinping wa China amekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyekuja China kuhudhuria Mkutano wa Baraza la tatu la Ushirikiano wa Kimataifa wa“Ukanda Mmoja, Njia Moja”.
Rais Xi amesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa lazima ifungamane na kuzingatia zaidi masuala ya maendeleo ambapo dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto na matishio mengi. Kutolewa kwa mawazo ya kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja, na Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja”(BRI) na Pendekezo la Maendeleo ya Dunia (GDI) ni kwa ajili ya kutafuta njia ya kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja na kuhimiza maendeleo ya pamoja ya nchi mbalimbali duniani, na pia ni kuunga mkono Ajenda 2030 ya Umoja wa Mataifa.
Rais Xi amesema Umoja wa Mataifa ni mwenzi muhimu katika ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” na China inapenda kushirikiana na shirika hilo kuhimiza ujenzi huo.
Bw. Guterres amesema pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” lililotolewa na rais Xi limetoa njia muhimu na yenye ufanisi katika kusaidia nchi zinazoendelea kupata maendeleo, na ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano wa Kusini-Kusini. Hatua nane alizotangaza rais Xi katika mkutano wa kilele wa mwaka huu zinalingana na malengo na madhumuni ya Umoja wa Mataifa, na shirika hilo linaishukuru China kwa kazi yake ya kulinda uhusiano wa pande nyingi wa kimataifa na litaunga mkono mapendekezo matatu yaliyotolewa na Rais Xi Jinping na kuendelea kuhimiza ushirikiano na China kwa kina.