Rwanda na CAF washirikiana kuendeleza soka na utalii barani Afrika
2023-10-19 14:43:30| cri

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Jumatano lilitangaza ushirikiano na serikali ya Rwanda, unaolenga kuendeleza soka na utalii barani Afrika kupitia Ligi mpya ya Soka ya Afrika (AFL) itakayoshirikisha klabu bora za soka barani humo.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB), ilisema AFL itakusanya timu kutoka kila nchi barani Afrika zikishindania taji kila mwaka kuanzia Oktoba 20, 2023 jijini Dar-es-Salaam, Tanzania.

"Ninafuraha kutangaza ushirikiano wetu na taifa ambalo linaonesha ari ya ukuaji na uwezo wa soka barani Afrika. Kwa pamoja, tutafungua upeo mpya wa mchezo huo mzuri katika bara letu, tukionesha mandhari yake ya kuvutia, utamaduni mzuri na mapenzi ya mashabiki wetu," Veron Mosengo-Omba, Katibu Mkuu wa CAF, alisema katika taarifa hiyo.

Naye Waziri wa Michezo wa Rwanda Aurore Mimosa Munyangaju, aliieleza ligi hiyo kama muungano mkubwa kwa bara la Afrika, na kuongeza kuwa ushirikiano huo unatoa fursa adimu kwa vijana wenye vipaji vya soka na ligi za ndani barani Afrika.