Serikali ya China imesema kuwa inaangalia fursa za uwekezaji kwenye nyanja ya kilimo na viwanda iliyopo mkoani Kigoma ili kuwezesha wafanyabiashara kutoka China kuwekeza Kigoma kutokana na fursa ya uwekezaji iliyopo mkoani humo.
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian alisema hayo alipokutana na Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye ofisini kwake na kusema kuwa amevutiwa na hali ya hewa ya Kigoma ambayo inaonekana kuwa na tija kubwa katika suala la kilimo ambapo mazao ya aina mbalimbali yanastawi.
Alisema kuwa mpango huo unalenga kuimarisha uhusiano wa kindugu uliopo baina ya China na Tanzania ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mao Ze Dong wa China ambao umefanya nchi hizo kushirikiana kwa karibu kwenye mambo mbalimbali.
Andengenye alimwambia Balozi Chen kuwa serikali kwa sasa inaufanya Mkoa wa Kigoma kama mkoa wa kimkakati katika kukuza uchumi hasa kutumia soko lililopo nchi za maziwa makuu, hivyo kwa sasa mkoa huo unakaribisha wawekezaji wakubwa na wadogo kuona namna wanavyoweza kutumia fursa hiyo kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.