Wataalamu wa Tehama wahimiza matumizi ya teknolojia ya 5G barani Afrika kwa ajili ya ukuaji wa uchumi
2023-10-20 09:01:20| CRI

Wataalamu wa Tehama (ICT) waliohudhuria Kongamano la mawasiliano ya mtandao wa Internet duniani 2023 (MWC2023) linalofanyika mjini Kigali, wamesema nchi za Afrika zinahitaji kuimarisha na kuharakisha juhudi za kuendeleza mtandao wa 5G katika bara zima ili kuleta mapinduzi ya kiviwanda, kuimarisha muunganiko, na kuendeleza ukuaji wa uchumi.

Kongamano hilo lililofanyika Oktoba 17-19, liliwaleta pamoja zaidi ya wajumbe 2,500, wakiwemo viongozi wa kisiasa na wadau wengine kutoka Afrika na dunia nzima.

Baadhi ya wataalam wamesema teknolojia ya 5G inatarajiwa kuchangia ukuaji wa Afrika kwa kuongeza nafasi za ajira na kuboresha mapato, kwani mfumo unaozunguka uchumi wa 5G una nguvu zaidi kuliko teknolojia nyingine zilizotangulia katika nyanja ya mawasiliano ya kidijitali.

Ofisa mkuu wa kampuni ya Huawei katika eneo la kusini mwa Afrika Bw. Li Tao amesema teknolojia ya 5G ina uwezo mkubwa wa kuhimiza maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.