Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeahidi kuiunga mkono Tanzania kwenye utekelezaji wa mpango wake wa kilimo unaolenga kupanua ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu inasema mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu ametoa ahadi hiyo Jumatano wiki hii wakati alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kando ya mkutano wa Jukwaa la Chakula Duniani uliofanyika Rome, nchini Italia.
Bw. Qu amesema FAO imevutiwa na mpango wa serikali ya Tanzania uitwao “Building a Better Tomorrow” unaolenga kuwapa vijana waliochaguliwa ekari 10 za ardhi kila mmoja kwa shughuli za kilimo, na FAO itaunga mkono mpango huo unaolenga kuwawezesha vijana na wanawake kwenye sekta ya kilimo.