Maonesho ya Uagizaji na Mauzo ya Nje ya China yavutia waoneshaji na wanunuzi kutoka kote duniani
2023-10-20 09:00:34| CRI

Maonesho ya 134 ya Uagizaji na Mauzo ya Nje ya China, ambayo yanajulikana kama ‘Canton Fair’, yalifunguliwa Jumapili huko Guangzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Guangdong kusini mwa China. Maonesho haya yatakayoendelea hadi Novemba 4, yamevutia waoneshaji na wanunuzi kutoka kote duniani. Kwa mujibu wa msemaji wa maonesho hayo Xu Bing, zaidi ya wanunuzi 100,000 kutoka zaidi ya nchi na maeneo 200 wamejiandikisha kwa ajili ya tukio hilo. Ameelza kuwa jukwaa la mtandaoni la maonesho hayo litatoa huduma kwa waoneshaji na wanunuzi.

Yakilinganishwa na maonesho yaliyopita, eneo la maonesho ya mwaka huu limepanuliwa kwa mita za mraba 50,000 na idadi ya mabanda ya maonesho pia itaongezeka kwa karibu 4,600.

Zaidi ya waoneshaji 28,000 watashiriki katika tukio hilo, ikijumuisha biashara 650 kutoka nchi na maeneo 43. Maonesho hayo yaliyozinduliwa mwaka 1957 na kufanyika mara mbili kwa mwaka, yanachukuliwa kuwa kipimo kikuu cha biashara ya nje ya China.

Wakati huohuo zaidi ya wafanyabiashara 95 wa Tanzania watashiriki maonesho mafunzo ya wajasiliamali katika monesho hayo ya ‘Canton Fair’ kupitia Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania.

Akifafanua zaidi juu ya safari hiyo, Mkurugenzi wa TWCC, Mercy Sila amesema lengo la safari hiyo ni kuwawezesha wajasiliamali hao kupata fursa za kimataifa, ambapo wataweza kujionea mashine za viwanda, vipodozi, mavazi, mashine za kilimo au mashine za kutengeneza chakula. Alisema mategemeo makubwa ya safari hiyo ni kuhakikisha kwamba wafanyabiashara hao wakirudi watakuwa sio sawa na wale waliondoka kwakuwa biashara zao zitakuwa na kuchangia katika kukua kwa uchumi.

Na habari nyingine zinasema pato la ongezeko la thamani la viwanda la China, ambalo ni kiashiria muhimu cha uchumi, lilipanda kwa asilimia 4 mwaka hadi mwaka katika robo tatu za kwanza za mwaka huu.

Hii ni kulingana na data kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Mwezi Septemba pekee, pato la viwanda lilipanda kwa asilimia 4.5 mwaka hadi mwaka, kulingana na NBS.