Mjumbe maalum wa China anayeshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati balozi Zhai Jun, amesema njia ya msingi ya kuondoa mzozo wa Palestina na Israel ni kutekeleza suluhisho la nchi mbili na kuanzisha taifa huru la Palestina.
Balozi Zhai ameyasema hayo katika mkutano wa amani wa Cairo ulioitishwa na Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri ili kupunguza mzozo wa Gaza. Amebainisha kuwa China inafuatilia kwa karibu hali ya mzozo wa Palestina na Israel na ina wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa kasi kwa mzozo huo, ambao umesababisha vifo na majeruhi ya raia wengi na msukosuko wa kibinadamu.
Amefahamisha kuwa China inalaani vitendo vyote vinavyodhuru raia, kupinga ukiukaji wowote wa sheria za kimataifa, na kuhimiza kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi zinazoweza kuchochea hali hiyo na kufunguliwa kwa njia za misaada ya kibinadamu. Balozi huyo pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa na busara na kutopendelea upande wowote kwenye suala la Palestina na kuchukua hatua madhubuti.
Zhai pia alipendekeza Umoja wa Mataifa uitishe mkutano wa kimataifa wa amani wenye mamlaka zaidi, ushawishi, na mpana zaidi ili kufikia makubaliano ya kimataifa juu ya kukuza amani, na kupata suluhisho la kina, haki na la kudumu katika suala la Palestina mapema iwezekanavyo.