Jeshi la Sudan lasema mazungumzo ya amani yataanza tena Jeddah, Saudi Arabia
2023-10-23 09:43:26| CRI

Jeshi la Sudan limesema litaanza tena mazungumzo ya amani na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) siku ya Alhamisi katika mji wa bandari wa Jeddah, Saudi Arabia.

Naibu kamanda wa jeshi la Sudan Shams-Eddin Kabashi alisema katika hotuba yake kwa maafisa wa jeshi katika kambi ya jeshi ya Wadi Seidna huko Omdurman kuwa wamepokea mwaliko wa kwenda Jeddah ili kuanza tena mazungumzo.

Vyombo vya habari nchini Sudan viliripoti kuwa Saudi Arabia na Marekani, ambazo zimekuwa zikipatanisha mazungumzo hayo tangu Mei, ziliweka tarehe 26 Oktoba kama tarehe ya kurejesha mazungumzo hayo. Mazungumzo hayo yalisitishwa mwezi Julai kutokana na tofauti za kimsingi kati ya pande zinazozozana.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Sudan, nchi hiyo imekuwa ikishuhudia mapigano makali kati ya jeshi na Kikosi cha Msaada wa Haraka mjini Khartoum na maeneo mengine tangu Aprili 15, na kusababisha takriban vifo 3,000 na zaidi ya majeruhi 6,000.