Mwanadiplomasia mwandamizi wa China atoa wito wa kuzuia mzozo kati ya Palestina na Israel usizidi kuongezeka
2023-10-24 09:50:26| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi Jumatatu alisema kuhusu mzozo unaoendelea kati ya Palestina na Israel, ni muhimu kuzuia hali hiyo isizidi kuongezeka na kusababisha matatizo makubwa zaidi ya kibinadamu.

Waziri Wang ameyasema hayo alipoongea kwa simu na mwenzake wa Israel Eli Cohen, ambapo Cohen alieleza msimamo wa Israel na wasiwasi wake wa kiusalama kuhusu mzozo kati ya Palestina na Israel. Bw. Wang amebainisha kuwa China ina wasiwasi mkubwa juu ya kuendelea kuongezeka kwa vita na hali inayozidi kuwa mbaya, na kusikitishwa sana na idadi kubwa ya vifo vya raia vilivyosababishwa na vita.

Amesema China inalaani vitendo vyote vinavyodhuru raia na kupinga ukiukaji wowote wa sheria ya kimataifa, na kuongeza kuwa nchi zote zina haki ya kujilinda, lakini zinapaswa kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kulinda usalama wa raia. Hivyo amesema maafikiano ya jumuiya ya kimataifa ni kuwepo kwa suluhu ya nchi mbili.

Wakati huohuo Bw. Wang alipoongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyad Al–Maliki, amefafanua kuwa inachohitaji zaidi Ukanda wa Gaza ni juhudi za kuleta amani, usalama, chakula na dawa, badala ya vita, silaha na risasi ama hesabu za kijiografia.