Upatanishi wa kuwaachilia huru mateka wenye uraia wa nchi mbili wanaoshikiliwa na Hamas unaendelea
2023-10-24 09:52:14| CRI

Chanzo nchini Palestina kimetangaza kwamba upatanishi unaoongozwa na Qatar, pamoja na ushiriki wa Misri na Umoja wa Mataifa, kwa sasa unaendelea ili kuharakisha makubaliano ya taratibu za kuachiliwa huru mateka wenye uraia wa nchi mbili wanaoshikiliwa na kundi la Hamas, ili kupunguza mgogoro wa umwagaji damu kati ya Hamas na Israel.

Chanzo hicho, kilichotaka jina lake kutotajwa kiliambia shirika la habari la China Xinhua kwamba Hamas iko tayari kusimamia operesheni hiyo, kwa sharti kwamba Israel itapunguza mashambulizi yake kwenye ukanda wa Gaza, ili kuhakikisha mchakato wa kuwaachilia mateka. Chanzo hicho kilikataa kuzungumzia idadi na ni mateka wenye utaifa gani wanaokusudiwa kuachiliwa. Vikosi vya Al-Qassam, mrengo wenye silaha wa Hamas, vilitangaza wiki iliyopita kwamba idadi ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa ni kati ya 200 na 250.

Tarehe 7 Oktoba, Hamas ilianzisha mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya Israel yanayojulikana kama "Mafuriko ya Al-Aqsa," kwa kurusha maelfu ya makombora ya roketi na kujipenyeza kwa wapiganaji wa Palestina katika ardhi ya Israel.