Shilingi ya Kenya yaporomoka kwenye kiwango cha chini zaidi katika historia dhidi ya dola
2023-10-24 09:46:30| CRI

Shilingi ya Kenya Jumatatu iliporomoka kwenye kiwango cha chini zaidi katika historia cha 150 dhidi ya dola ya Marekani, na kuongeza shinikizo katika kupungua kwa hifadhi ya fedha za kigeni nchini humo jambo ambalo linafanya uagizaji bidhaa kuwa wa gharama za juu zaidi kufuatia ongezeko la mfumuko wa bei.

Benki Kuu ya Kenya (CBK) iliuza dola moja kwa shilingi 149.94 jana Jumatatu, ikipungua kwa asilimia 24 ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita.

Akiba ya fedha tarehe 19, Oktoba ilifikia kiwango cha chini zaidi cha dola za Kimarekani bilioni 6.83, ambazo zilitosha kuagiza bidhaa kutoka nje kwa miezi 3.67, ikishuka kutoka dola bilioni 7.29 mwaka mmoja uliopita.

Benki kuu, katika ripoti yake mpya iliyotolewa Oktoba 15 ya uthabiti wa sekta ya fedha, ililaumu kudhoofika kwa sarafu ya nchi hiyo kutokana na "kuimarika kwa kasi kwa sera ya fedha katika nchi zenye maendeleo makubwa ya kiuchumi, zikilazimisha viwango vya riba vya kimataifa kupanda, na kusababisha wawekezaji kukimbilia sarafu zenye ubora kama dola."