Nchi wanachama wa BRICS wakubali kuzidisha ushirikiano ili kuhimiza ufufukaji endelevu wa utalii
2023-10-25 10:14:51| CRI

Nchi wanachama wa BRICS zikiwa ni pamoja na Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini Jumanne zilikubaliana kuzidisha ushirikiano ili kutimiza ufufukaji endelevu na jumuishi kwenye sekta ya utalii.

Nchi hizo zimeeleza hayo katika taarifa iliyosainiwa kwenye mkutano wa mawaziri wa utalii wa nchi za BRICS uliofanyika Jumanne mjini Cape Town. Mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Ufufukaji endelevu na jumuishi kwenye sekta ya utalii” utaendelea kwa siku tatu hadi tarehe 26 Oktoba.

Taarifa hiyo ilisema nchi wanachama wa BRICS zinatambua athari kubwa zilizotokana na janga la COVID-19 kwenye sekta ya utalii, lakini janga hilo pia limeleta fursa ya kutekeleza mageuzi wakati sekta ya utalii inatengeneza mustakabali imara na jumuishi zaidi. Kutimiza ufufukaji endelevu na wa kijani kwenye sekta ya utalii kunahitaji kufuatilia zaidi sera imara na endelevu za mazingira na utamaduni wa kijamii.