Washiriki wa Kongamano la Abuja waona “Ukanda Mmoja, Njia Moja” umeiletea Afrika fedha na teknolojia zinazohitajika
2023-10-25 08:41:36| CRI

Matunda mengi yaliyopatikana katika Mkutano wa Kilele wa Baraza la tatu la Ushirikiano wa Kimataifa la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” yamefuatiliwa na kupongezwa barani Afrika.

Mjumbe mwandamizi wa Pendekezo la Kunyamazisha Silaha (“Silencing the Guns”) la Umoja wa Afrika Bw. Mohamed Ibn Chambas amesema, chini ya mfumo wa ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” kati ya China na Afrika, misaada ya China kwa Afrika na biashara kati ya pande hizo mbili imeongezeka kwa kasi, na ushirikiano kati ya Afrika na China umeiletea Afrika fedha na teknolojia zinazohitajika sana.

Bw. Chambas amesema hayo kwenye mkutano wa nne wa Kongamano la Abuja uliofanyika hivi karibuni, ambao uliandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang na Taasisi ya Gusau ya Nigeria. Kwenye mkutano huo, Bw. Chambas alikanusha shutuma zilizotolewa na baadhi ya nchi za Magharibi zinazodai kuwa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” umeiwekea Afrika kile wanachokiita “mtego wa madeni”, akisema shutuma hizo hazina msingi wowote. Takwimu zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya madeni ya nje ya Afrika yanatoka  mashirika ya kifedha ya pande nyingi na watoaji mikopo ya kibiashara, na wala sio China. Uwekezaji na jitihada zilizofanywa na China barani Afrika vinasaidia kuijenga kuwa bara lenye amani na ustawi zaidi.

Mwenyekiti ya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Miundombinu ya Nigeria na Kampuni ya Bima ya Nicon Bw. Lamis Dikko anaona, ujenzi wa pamoja wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” utachangia maendeleo ya miundombinu nchini Nigeria na kutatua tatizo la upatikanaji wa fedha. Kwenye mchakato huo, Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ni muhimu sana, kwa kuwa mfumo wenye ufanisi wa ikolojia ya kifedha unahitajika kuleta pamoja wadau wengi zaidi na kutumia nyenzo nyingi zaidi za kifedha, ili kukidhi mahitaji ya fedha ya muda mrefu kwenye miradi ya miundombinu.