Mwakilishi wa China ataka kusimamisha vita mara moja kati ya Palestina na Israel
2023-10-25 10:17:08| CRI

Mwakilishi wa kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa balozi Zhang Jun ametoa wito wa kusimamisha vita kati ya Palestina na Israel, akisema huu ni wito uliotolewa na jumuiya ya kimataifa.

Akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati likiwemo suala la Wapalestina jana, balozi Zhang pia alilitaka Baraza la Usalama litumie lugha iliyo wazi na isiyo na mashaka ya kutaka kusimamishwa kwa mapigano haya mara moja.

Amesema ni lazima ifahamike kwamba kuruhusu mapigano huko Gaza yaendelee kwa visingizio vyovyote vile, hakutaleta ushindi kamili wa kijeshi kwa pande zote mbili, bali kuna uwezekano mkubwa wa kusababisha maafa ambayo yataathiri kanda nzima, kuondoa kabisa matarajio ya suluhu ya nchi mbili, na kuwatumbukiza watu wa Palestina na Israel katika mzunguko wa chuki na makabiliano ya kudumu.

Ameongeza kuwa nchi mbalimbali zinapaswa kuzingatia maadili, badala ya kung'ang'ania hesabu za siasa za kijiografia, pamoja na vigezo viwili. Baraza la Usalama lazima lifanye kila liwezalo kuleta amani, badala ya kutumia lugha ya utatanishi au kukubali hali kuzidi kuwa mbaya na raia wengi zaidi kukabiliana na tishio la kifo.