UM wasema usalama wa chakula unaimarika nchini Kenya huku ukame ukipungua
2023-10-25 10:11:26| CRI

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema hali ya usalama wa chakula nchini Kenya inaimarika huku ukame uliosababishwa na ukosefu wa mvua kwa misimu minne mfululizo ukipungua.

Akiongea na Shirika la Habari la China, Xinhua, huko Nairobi nchini Kenya, Mwakilishi wa FAO nchini Kenya Carla Mucavi, alisema idadi ya watu wasio na chakula imepungua kutoka milioni 4.8 hadi wastani wa watu milioni 1.5, wengi wao wakiwa katika kaunti kame na nusu kame.

Mucavi alisema kuanza kwa msimu wa mvua za Oktoba hadi Disemba unatarajiwa kuboresha zaidi hali ya usalama wa chakula nchini humo kwani wakulima watapata mavuno mengi.

Alibainisha kuwa FAO imeshirikiana na serikali ya Kenya na wafadhili ili kuimarisha hatua za ustahimilivu wa jamii zilizoathiriwa na ukame. Hatua hizi ni pamoja na kutoa chakula cha mifugo, kutoa chanjo kwa mifugo, na kutoa fedha taslimu kwa wafugaji ili kuongeza usalama wa chakula.