Tanzania yawataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi
2023-10-25 10:10:26| CRI

Serikali ya Tanzania imewataka vijana kuweka ajenda ya mazingira katika vipaumbele vyao ili kusaidia nchi kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo amesema Serikali imeazimia kuwezesha na kukuza sauti za vijana ambao wana nafasi ya kipekee ya kuendesha mipango ya ubunifu na yenye matokeo inayokabili changamoto za hali ya hewa nchini.

Aliyasema hayo alipokuwa akifungua semina ya siku moja ya kufungua fursa za vijana ili waweze kushiriki kikamilifu katika Mpango wa Kitaifa na Kimataifa wa Kupambana na Mabadiliko ya Hali ya Hewa, iliyoandaliwa na “Youth for Climate Action Tanzania” mjini Dodoma.

Amesisitiza kuwa vijana wana kila sababu ya kuendesha ajenda ya maendeleo na kupendekeza kila hatua zinazowezekana ili kuepusha athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi tayari zimeanza kushuhudiwa nchini kote, zikiathiri kilimo, rasilimali za maji, afya na mifumo ya ikolojia.